Watoto wa kike/mabinti wanakumbwa na changamoto mbalimbali katika mazingira tunayoishi, miongoni mwa changamoto hizo ni ukatili wa kijinsia, mimba zisizotarajiwa, ndoa za utotoni, kukosa mentors (walimu wa kuwaongoza) na mahusiano yasiyo sahihi. Endapo binti atakosa mwongozo sahihi anaweza kushindwa kutimiza ndoto zake au akatimiza chini ya kiwango alichotegemea.

 

Wanafunzi wa shule ya Sekondari Tomondo wakipata elimu

GESGEMO imekuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia watoto wa kike/mabinti kutimiza malengo yao. Miongoni mwa mambo ambayo GESGEMO imekuwa ikiyapa kipaumbele ni kutoa elimu juu ya  kujitambua, kujitunza, na kujithamini. GESGEMO ilishirikiana na mradi wa GWAP, Girls with a Purpose kutoa elimu hii katika shule ya Sekondari Tomondo wilaya ya Morogoro vijijini mkoani Morogoro.

Kwa nini Kujitambua? Kwa maana nyepesi kujitambua ni kujifahamu, kujijiua au kujielewa. Kwa maana hiyo kujitambua ni hali au uwezo wa mtu kufahamu na kujielewa yeye ni nani, ana majukumu gani, anastahili nini na yapi afanye kwa wakati gani na mazingira gani.

Kujitambua kunaweza kuwa kwa namna tofauti tofauti kama vile kujitambua kihisia, kimwili, kiuchumi, kimazingira na kiuwezo.  Mabinti wanapojitambua huweza kuwa na maamuzi sahihi na kusimamia ndoto zao kwa ujasiri

Kwa nini kujithamini?  Kujithamini ni Imani chanya kuhusu mtu mwenyewe pamoja na hisia zake. Mabinti wanapojithamini wanakuwa na misingi wanayoisimamia na hawataruhusu mtu kuwavunjia heshima. Kujithamini kunawasaidia mabinti kukabiliana na changamoito zozote wanazokutana nazo kwa njia sahihi pasipo kuuza utu wao.

Kwa nini Kujitunza? Kujitunza ni muhimu kwa afya ya na kimwili na kiakili kwa mabinti. Ni pamoja na kula lishe bora, kutokutumia madawa na kulevya, pombe na mengineyo yanayoharibu afya, kufanya mazoezi, kuwa wasafi, kupumzika n.k. Mabinti wanapojitunza na kujijali huweza kuwa na afya njema na uwezo mzuri wa kufikiri.

Igizo maalum lilioandaliwa ili kuwapa wazazi, walimu na wanafunzi uelewa juu ya mada iliyokuwa ikifundishwa

Ili mabinti waweze kujitambua, kujithamini na kujitunza, jamii kwa ujumla inaweza kuwasaidia kwa kufanya yafuatayo: Kuwapa mabinti mifano chanya ya watu waliofanikiwa na wanaoweza kuwapa hamasa ya kuendelea mbele zaidi, kuwapa mabinti fursa mbalimbali za kujifunza na kuwajengea uwezo, kuwalinda dhidi ya unyanyasaji, kuwajengea ujasiri na kujiamini pamoja na kuwatia moyo katika kupiga hatua zaidi.

Tulipata fursa pia ya kuzungumza na wazazi wa wanafunzi hawa pamoja na watoto wa kiume kwa kuwa na wao ni sehemu kubwa ya kumsaidia mtoto wa kike kufikia malengo yake

Baadhi ya wazazi wa wanafunzi wa shule ya Tomondo

Kuwekeza katika kujitambua, kujitunza, na kujithamini kwa mabinti, kutasaidia waweze kufikia malengo yao na kuwa na msaada chanya katika jamii.